Tuesday, February 9, 2016

UCHAMBUZI.JUA LA MAWIO NA MACHWEO HUFANANA TUTAZAME MASHARIKI

Umewahi kujiuliza kuwa endapo utapoteza fahamu ikiwa ndio kwanza jua linachomoza (kwa watu wa magharibi watanielewa zaidi) kisha ukazinduka jioni wakati jua linaelekea kuzama, nini kitatokea? Unaweza kudhani kuwa muda haujakwenda tangu ulipopoteza fahamu, mpaka akili itakapotulia na ukatambua mashariki ni wapi na magharibi ni wapi. Miaka kadhaa iliyopita mimi na familia yetu tulisafiri kwenda kwenye maziko ya marehemu mama mkubwa (mama yake babu yangu), maeneo ya mcharo wilaya ya bunda. Baada ya shughuli ile, asubuhi iliyofuata tulifanya safari kwenda kijiji kingine kumsalimu dada wa marehemu, nakumbuka vyema kuwa nilikuwa mgonjwa kiasi wakati ule. Nilikuwa nafurahia zaidi mwangaza ule wa jua la asubuhi unavyoonekana katikati ya majani marefu upande wa mashariki. Usingizi ulinipitia na nilipokuja kushtuka tulikuwa tumekwisha fika na niliamshwa kwa ajili ya chakula. Macho yangu haraka nikayakimbiza kwenye jua na nikaona rangi ile inayonivutia ikiwa inaangaza, sikushituka mpaka niliposikia mtu akisema kuwa ni saa 11 jioni na hapo ndipo nilitambua jua limekwenda magharibi haliko tena mashariki.

Japo jua la mawio na machweo yote hutupatia Vitamin D lakin yana tofauti kubwa. Unapoona jua la mawio ni dalili kuwa unaanza siku mpya na unao wakati wa kuyatengeneza mafanikio yako ya siku hiyo na pengine ya baadae, hapa ndipo tunapozidiana ujanja, katika matumizi ya huu muda tuliopewa. Eneo hili la matumizi ya fursa ndio linamtofautisha Messi na Sadio Mane, hapa utaiona tofauti kati ya Chicharito na Sturridge. Kila kiumbe kimepewa masaa 24 ya kuishi kila siku, ni kama tumepewa mtaji wa kuanzia ni wewe unaamua uwekeze wapi, kwenye biashara ya nyanya ili uingize kidogo kidogo utengeneze mtaji wa biashara ya magari au unaamua kuwekeza kwenye vyote viwili kwa mtaji mdogo ulionao na unaamini kuwa utaweza kuvimudu. Matokeo ya kuwekeza katika vyote viwili ni kuwa biashara hizo zitakufa moja baada ya nyingine na utaanza tena kutengeneza mtaji wa kuanza biashara nyingine. Hii nyingine nayo bila mkakati madhubuti itakufia mikononi.

2019 inaweza kuonekana mbali sana kwa matamshi lakini ki mahesabu imeshafika na iko mlangoni. Ninapouwaza mwaka 2019 moja kwa moja kwenye akili yangu linakuja neno U17 (under 17), labda ni kwakuwa sijawahi kushuhudia nchi yangu ikiaandaa michuano mikubwa ya soka zaidi ya CECAFA SENIOR CHALLENGE, au ni kwakuwa sijaona timu yangu ikishiriki fainali za michuano mikubwa zaidi ya CHAN, ambayo nayo tuliishia raundi ya kwanza. Naisubiri kwa hamu 2019 ili niweze kushuhudia yote hayo mawili yakitukia kwa pamoja. Lakini swali ni je, tutafika wapi kaka wenyeji? Je, huu utakuwa ni mwanzo wa sisi kwenda kucheza fainali za kombe la dunia? Ama itakuwa ni bonanza? Je, itakuwa ni njia ya kuelekea kushuhudia majina ya wachezaji wa nchi yangu kwenye nyuz nyeupe za Real Madrid ama yatabaki kwenye nyuzi za Azam, Simba , Yanga na pengine Mwadui?

Wakati nikitafakari haya najiuliza kuna mkakati mkubwa unaoonekana wa kujiandaa na haya? Kuna Jua la mawio na jua la machweo, sijui ni kwasababu tulipoteza fahamu na tumezinduka tukakuta yote yako angani sasa tunashindwa kutambua lipi ni lipi kwa kuwa yanafanana rangi! Ingekuwa ni amri yangu ningeomba kuipumzisha kwanza Taifa stars kushiriki mashindano ya kimataifa ama kama hilo sio bora basi ningeiacha iendelee na utaratibu huo lakini nguvu yangu kubwa nikaielekeza kwa timu ya U13 ambayo niliishuhudia Morogoro na mara ya mwisho niliisikia iko Tanga, ukiniuliza ilipo leo sifahamu. Hili ndio jua letu la mawio, huku ndio kuna samaki wabichi tunaoweza kuwakunja. Hawa wengine wa jua la mawio hata tukiwakunja mkia utabaki nje tu, mwisho wa siku wapita njia watawavuta nje ya chombo kama ilivyozeleka. Ni ajabu sana kuona wanaopaswa kutushika mkono na kututazamisha mashariki nao  wanatazama magharibi na wengine bado hawajazinduka kabisa. Nani wa kumfunga paka kengele? Nani atatumbua hili jipu?

Natamani waTanzania wote tulie machozi ili kuwaokoa akina Juma Kaseja, akina Nadir Haroub na akina Samatta wa miaka ijayo. Nilishasema kuwa Tanzania ni msitu mkubwa sana wa vipaji kiasi kwamba vipaji ambavyo havijakomaa tunashindwa kuvitambua maana bado tunashangaa vile vilivyokomaa. Macho yetu bado hayajachoka kuona maujanja ya Ibrahim Ajib, tunatamani kuendelea kumshuhudia Farid Mussa na bado masikio yetu yana hamu ya kusikia habari za Samatta na akina Mwaishuya. Tahamaki tahamaki 2019 imekwishafika na timu yetu ambayo ndio itakuwa mwenyeji hatujaiandaa kwa kuzikabili timu zitakazokuja. Mwaka jana wakati tangazo lile linatoka nikaona hatua za wazi zikichukuliwa na nikajua ule ni mwendo wa ku 'troti' nikaamini kuwa mwili utakapopata moto tutaanza kukimbia cha ajabu naona kama hata ku 'troti' tumeacha sasa hivi tunatembea kabisa tena mwendo wa kutoka shambani. Ukistaajabu ya Azam kuvuruga ratiba ya ligi utayaona ya U13 kusahau mipango ya kuelekea 2019.

Tumewaona Rwanda kwenye CHAN, waliyoyafanya ni macho na video ndio vitasimulia. Tumewaona Mauritius wakitupiga kule kwenye COSAFA. Tunatamani kuwafunga Algeria na Nigeria,tunatamani kuwa Spain lakini tunaizingatia jioni sana kuliko kuizingatia asubuhi yetu ya kesho. Kama tutaendelea hivi basi itatuchukua miaka zaidi ya 20 tena kumshuhudia Samatta mwingine. Hebu tutafute makabrasha ya Ghana, Mali na Germany. Ili tujue walikotoka akina Ayew, Bakayoko, Keita, Muntari na akina Gotze na Ozil. Ni kweli vipaji tunavyo vingi kiasi kwamba tunashindwa kuchagua pa kuzingatia, na ni kweli kabisa kuwa jua la mawio na machweo hufanana rangi, lakini tutazame mashariki zaidi kuliko magharibi, maana huko ndio kuna matumaini ya asubuhi.

GULINJA E. GASPER

No comments:

UTAWALA WA KIHASPANIOLA KATIKA SOKA LA ULAYA

WAHISPANIA WAMETAWALA SOKA LA ULAYA.WAKATI WA KUJIULIZA Msimu uliopita Seville walitwaa ubingwa wa Ueropa league kwa kuifinga Liverpool 3-1...